KATIBA YA CHAMA CHA
MSHIKAMANO NA
MAENDELEO YA NKUNGI
NA VIJIJI JIRANI
KATIKA WILAYA MPYA YA
MKALAMA, MKOANI SINGIDA
YA JAMII INAYOISHI DAR
ES SALAAM
(Toleo la Pili)
1) UTANGULIZI
Ili kuimarisha umoja wa
wanajamii wa Nkungi na Vijiji Jirani vya Nduguti, Nkalakala, Mwando, Mwanga, Kidarafa,
Mng’anda, Malaja, Singa, Ilunda, na Iambi
katika wilaya mpya ya Mkalama waishio
Dar Es Salaam, tumeamua kwa hiari na kwa dhati bila kulazimishwa na mtu yeyote kuanzisha
Kikundi cha Umoja wetu yaani CHAMA.
2) JINA LA CHAMA
Jina
la Chama litakuwa Mshikamano na
Maendeleo ya Nkungi na Vijiji Jirani ya Jamii Inayoishi Dar Es Salaam (kwa kifupi: Kwilae Social Development
Group). Jina Mshikamano na Maendeleo lina maana ya kushirikiana kwa dhati
kama familia moja inayoishi Dar Es Salaam kwa shida na raha, yaani kuwa na
umoja unaofungamana kwa dhati unaoudumisha upendo,ushirikiano, kufarijiana na
pia kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Jamii inayoishi Nkungi na Vijiji
Jirani katika wilaya ya Mkalama mkoani Singida. Anwani ya chama itakayotumika
itakuwa kama ifuatavyo: Private Bag 70612, DAR ES SALAAM.
3) MADHUMUNI YA CHAMA
a) Kuwa
na Mfuko utakaosaidia wanachama kuwa na mshikamano,
b) Kuunganisha
wanajamii wa Nkungi na Vijiji Jirani waishio Dar Salaam;
c) Kutoa
msaada utakaoidhinishwa kwa mwanachama ambaye amepatwa na msiba au kuumwa sana;
d) Kushiriki
katika shughuli za maendeleo ya Nkungi na Vijiji Jirani kama zitakavyopitishwa
na jamii hiyo.
4) SIFA ZA MWANACHAMA
a)
Ni yule ambaye anaipenda
kwa Dhati Nkungi na Vijiji Jirani;
b)
Awe na umri usiopungua miaka kumi na nane (18);
c)
Ni yule ambaye anajitegemea na ana akili timamu;
d)
Ni yule ambaye anaishi Dar Es Salaam na ambaye wazazi/ ndugu zake
wanaishi Nkungi na Vijiji Jirani;
e)
Ni yule ambaye anaweza kusoma na kuandika. Awe tayari kuielewa,
kuitetea na kutekeleza masharti yote ya uanachama;
f)
Ni yule ambaye anaishi nje ya Dar Es Salaam na
amependa kuendelea kuwa mwanachama kwa kutimiza masharti yote ya chama yaliyomo
kwenye Katiba;
g)
Yule anayetoka nje ya Dar Es Salaam na anatoka katika vijiji husika
(Aya Na. 1).
5) HAKI ZA MWANACHAMA
a) Kushiriki
kikamilifu katika awamu zote za uchaguzi wa viongozi wa chama;
b) Kupata
huduma za umoja kama ilivyoainishwa katika
Katiba;
c) Kuwania
kuchaguliwa katika nafasi yoyote ya uongozi wa chama isipokuwa mwanachama
anayeishi nje ya Dar Es Salaam;
d) Kutoa
mapendekezo, malalamiko au kudai mabadiliko ili kudumisha chama. Atafanya hivyo
kwa maandishi na kuyafikisha kwa Katibu wa Chama.
e) Kujua
maendeleo ya chama;
f) Kuidhinisha
mipango na bajeti ya chama; na
g) Kuomba
kujitetea endapo amefanya kosa, kusimamishwa au kufukuzwa uanachama au uongozi
ili kuondolewa au kupunguziwa adhabu.
6) MAPATO YA CHAMA
Mapato ya Chama yatapatikana kwa
njia zifuatazo:
a)
Hisa za kila mwanachama kwa mwaka;
b)
Ada
ya kila mwezi;
c)
Michango ya rambirambi;
d)
Ruzuku; na
e)
Michango mbalimbali kama
itakavyopitishwa na wanachama.
7) KUJIUNGA NA CHAMA
Ili
kukiwezesha Chama kufanya kazi zake ipasavyo, kila mwanachama atalazimika
kuchangia Mfuko wa Chama kama ifuatavyo:
a)
Kujaza fomu maalum ili kujiunga na Chama kwa shilingi 5,000/=; na
b)
Kulipa kiingilio cha
uanachama shilingi 100,000/= (laki moja) kama
hisa.
Hata hivyo, viwango hivyo vya
michango vinaweza kubadilika kulingana na mahitaji ya wakati husika. Mapato
hayo yatawekwa katika Akaunti Maalum itakayofunguliwa kwenye Tawi la Benki
linaloruhusu kutoa kiasi kinachoweza kukidhi mahitaji yanayokusudiwa na
wanachama.
8) UTUNZAJI WA FEDHA ZA CHAMA
a)
Fedha za Chama zitatunzwa katika Benki iliyochaguliwa
na wanachama. Fedha za Chama zitatolewa benki kwa idhini ya wajumbe
walichagulia na wanachama;
(i)
Mhasibu;
(ii) Katibu;
(iii) Katibu
Msaidizi; na
(iv) Mjumbe
aliyechaguliwa.
b)
Benki statement ya akaunti ya Chama itawasilishwa
katika Mkutano Mkuu kwa uchambuzi kila baada ya miezi mitatu;
c)
Hesabu za Chama zitakaguliwa kila baada ya miezi
mitatu (3) na taarifa kuwasilishwa katika kikao cha pamoja kati ya kamati ya
usalama na kamati ya utendaji;
d)
Taarifa ya ukaguzi na maoni ya kamati ya utendaji
itawasilishwa na kuthibitishwa na Mkutano Mkuu;
e)
Taarifa itakapokubaliwa na mkutano mkuu itasainiwa;
f)
Ili
kuwawezesha wanachama kiuchumi katika siku za usoni, Chama kitatafakari kwa
kina namna ya kuwawezesha wanachama kiuchumi; na
g)
Endapo Kamati ya Usalama itathibitisha kwamba fedha za
Chama zimepotea, mhusika au mtunza hazina atazirudisha haraka kwa mujibu wa
kanuni za Chama la sivyo michango yake itafidia upotevu huo.Endapo kiasi
kilichoibiwa ni kikubwa ikilinganishwa na akiba ya mwanachama kwenye akaunti ya
chama, itabidi wanachama wachukue mali yoyote ya mtuhumiwa ambayo anayo
nyumbani kufidia kiasi cha fedha kilichoibiwa na mtuhumiwa ashitakiwe
mahakamani.
9) WAJIBU WA MWANACHAMA
a)
Kushiriki kwa kujituma katika shughuli zote
zinazolenga kufanikisha madhumuni ya Chama;
b)
Kutekeleza kwa uadilifu na nidhamu majukumu
atakayopangiwa katika kutekeleza madhumuni ya Chama;
c)
Kulipa ada ya kila mwezi shilingi 10,000/=;
d)
Kuchanga fedha za rambirambi zisizopungua shilingi
10,000/= kila tukio; na
e)
Kumchangia mwanachama anayeoa/olewa kiasi
kisichopungua shilingi 10,000/= (elfu kumi).
10) UENDESHAJI WA SHUGHULI ZA CHAMA
Shughuli za
chama zitaendeshwa na viongozi wafuatao:
a)
Mwenyekiti;
b)
Makamu Mwenyekiti;
c)
Katibu;
d)
Katibu Msaidizi; na
e)
Mweka Hazina.
Ili viongozi waweze kutekeleza
majukumu yao kikamilifu, kutakuwa na Kamati
zifuatazo ambazo zitawasaidia viongozi hao kutekeleza majukumu yao kikamilifu:
a)
Kamati ya Utendaji (wajumbe 17);
b)
Kamati ya Nidhamu na Usalama (wajumbe 5); na
c)
Kamati ya Matukio (wajumbe 7).
MAJUKUMU YA KAMATI MBALIMBALI ZA CHAMA
a) Majukumu ya Kamati Kuu ya Utendaji
Kwa
ujumla, Kamati Kuu ya Utendaji ni uongozi, yaani inaongozwa na Mwenyekiti;
Mwenyekiti Msaidizi; Katibu; Katibu Msaidizi; na Mtunza Hazina. Majukumu ya
Kamati hii yatahusu uendeshaji, usimammizi na uratibu wa shughuli za kila siku
za Chama ikiwa ni pamoja na:
(i) Kutunza
fedha na mali
zote za Chama;
(ii) Kutunza
shughuli za Chama na kumbukumbu za wanachama;
(iii)Kuandaa
ratiba za mikutano na vikao vyote vya Chama;
(iv)Kusimamia
utekelezaji na marekebisho ya Katiba;
(v) Kubuni
na kusimamia mikakati ya kuendeleza Chama; na
(vi)Kusimamia
utekelezaji wa maamuzi ya wanachama.
10.1 Katika
hali ya kawaida kamati ya utendaji itakutana mara moja kwa mwezi.
10.2 Mkutano
utaendeshwa na Mwenyekiti, kama hayupo Makamu Mwenyekiti atachukua nafasi yake.Iwapo
wote hawatakuwepo basi madaraka yao yataachwa kwa mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu ya Utendaji kuongoza kikao kwa
niaba yao.
10.3 Endapo
Katibu na Katibu Msadizi hawatakuwepo wajumbe watamchagua mjumbe mmoja kukaimu
nafasi hiyo.
10.4 Wajumbe
katika kamati hii watakaa madarakani kwa kipindi cha miaka mitatu (3).
11) MAJUKUMU YA VIONGOZI WA CHAMA
Kazi
za Mwenyekiti
(i)
Kiongozi mkuu wa chama;
(ii) Ataongoza
mikutano yote ya chama;
(iii) Kutoa
miongozo ya utekelezaji wa majukumu mbalimbali kwa mujibu wa taratibu za chama;
(iv) Kuratibu
mipango ya chama na kuidhinisha matumizi ya fedha za chama kwa mujibu wa
taratibu za chama; na
(v) Atawajibika
kwa mkutano mkuu wa chama.
Kazi
za Mwenyekiti Msaidizi
(i)
Atakuwa msaidizi na mshauri mkuu wa mwenyekiti;
(ii) Atafanya
kazi zote atakazopangiwa na mwenyekiti; na
(iii) Atawajibika
kwa mwenyekiti.
Kazi
za Katibu
(i)
Atakuwa ndiye mtendaji mkuu wa chama;
(ii) Atawajibika
kwa mwenyekiti na Kamati ya utendaji;
(iii) Kuitisha
na kuandaa agenda na kumbukumbu za mikutano;
(iv) Kupokea
maombi ya wanachama wapya na kuwasilisha kwa Kamati Kuu ya Utendaji ili
kupitishwa;
(v) Kutunza
Daftari la majina ya wanachama; na
(vi) Kupokea
hoja mbalimbali za wanachama na kuzifanyia kazi.
Kazi
za Katibu Msaidizi
Atafanya kazi zote atakazopangiwa
na Katibu.
Kazi
za Mweka Hazina
(i)
Kukusanya michango, kutunza fedha na kumbukumbu zake;
(ii) Kutoa
taarifa ya mapato na matumizi ya fedha za wanachama kwenye mikutano yote ya
chama na kuhakikisha fedha zote zimepelekwa benki;
(iii) Kuandaa
benki statement;
(iv) Atawajibika
kwa Kamati Kuu ya Utendaji na Mkutano Mkuu wa Chama;
(v) Kuandaa
orodha ya wadaiwa kila mwezi na kuwasilisha kwenye mkutano wa wanachama wote
kupitia Kamati ya Utendaji;
(vi) Kutoa
ushauri wa masuala yote ya fedha kwa wanachama na namna nzuri itakayosaidia
fedha kupatikana wakati wote zitakapohitajika;
(vii)
Atawajibika katika shughuli zote za kifedha na zingine
atakazopangiwa na mwenyekiti.
b)
Majukumu
ya Kamati ya Nidhamu na Usalama ni
kufuatilia mwenendo, nidhamu na utekelezaji wa shughuli zote za chama na
mwanachama.
c)
Majukumu
ya Kamati ya Matukio ni pamoja na kufuatilia kwa karibu matukio yote
ambayo yatawapata wanachama na kutoa taarifa haraka kwa viongozi na wanachama
kwa hatua zaidi za msaada.
12) MKUTANO MKUU WA CHAMA.
Kutakuwa na mkutano wa wanachama
wote kila baada ya miezi mitatu kuanzia Januari ya kila mwaka. Mkutano wa
Wanachama wote utahusika na mambo yafutayo.
a)
Kuchagua viongozi wa Chama iwapo muda umekwisha;
b)
Kuchambua mapendekezo ya Kamati Kuu ya Utendaji kuhusu
mwelekeo wa Chama kwa mwaka;
c)
Kurekebisha vipengele vya katiba kwa kadri ya mahitaji
ya nyakati; na
d)
Kupokea, kuchambua na kuidhinisha taarifa ya mapato na
matumizi ya Chama kwa mwaka.
Ili kufanikisha mikutano ya
Chama kufanyika kama itakavyopangwa, kuanzia asilimia
50 ya wanachama wote watakaohudhuria pamoja na wale waliotoa udhuru inatosha
kufungua na kuendesha mkutano. Aidha, vikao vya wanachama vitaamuliwa kidemokrasia
kwa kupiga kura na hoja zote lazima zipitishwe kwa zaidi ya asilimia 50 ya
wajumbe wote watakaohudhuria kikao husika.
13) MFUMO WA UENDESHAJI CHAMA
Wanachama kwa kiasi kikubwa watatekeleza shughuli zao
kwa kujitolea na kujituma. Hata hivyo, wanachama watagharamia yafuatayo:-
a) Uchapishaji
wa miniti za mikutano ya wanachama, kamati ya utendaji na mkutano mkuu; na
b) Vifaa
vya msingi vya uendeshaji wa Chama.
14) WAKAGUZI WA HESABU
a) Kamati
ya Nidhamu na Usalama ndio itafanya shughuli zote za ukaguzi wa hesabu kila
baada ya miezi mitatu (3);
b) Kamati
hii itakuwa na jumla ya wajumbe watano (5); na
c) Nakala
za mapato na matumizi pamoja na taarifa za wakaguzi wa fedha zitawasilishwa
kwenye Mkutano Mkuu na zinaweza kupatikana au kuwekwa bayana kwa wanachama wote
watakaozihitaji kuziona wakati wowote.
15) MATUMIZI YA MICHANGO
a)
Endapo mwanachama (mume au mke) amefariki, Mfuko wa
Chama utatoa shilingi 300,000/= (laki tatu) ili kumpa mfiwa mkuu na pia kila
mwanachama atachangia shilingi zisizopungua 10,000/= (elfu kumi tu) ili kumpa
mfiwa mkuu;
b)
Endapo mwanachama amefiwa na mtegemezi wake (Aya Na.
16), Mfuko wa Chama utatoa shilingi 200,000/= (laki mbili) ili kumpa mfiwa mkuu,
na pia kila mwanachama atamchangia mfiwa mkuu shilingi zisizopungua 10,000/=
(elfu kumi);
c)
Endapo kwa tukio baya mwanachama atakuwa amefariki,
familia yake itakuwa na hiari ya kumchagua mrithi wa hisa za marehemu au
uanachama, bila kujaza fomu upya ya maombi ya uanachama;
d)
Ikiwa kutakuwa na ndugu zaidi ya mmoja katika Chama na
ikatokea wamepatwa na msiba, basi Chama kitatoa msaada wa watu wawili tu wa
familia hiyo ambao watawachagua kupokea msaada huo. Na katika hao ndugu, endapo
mmoja wao amefiwa na mkwe wake, basi atakayepata msaada wa Chama ni mlengwa
mwenyewe tu na Chama hakitawajibika kutoa msaada zaidi ya mwanachama mmoja;
e)
Gharama za vikao zitagharamiwa na wanachama wenyewe,
vikao vitafanyika sehemu yoyote itakayopendekezwa na wanachama;
f)
Kuchangia katika shughuli za maendeleo ya jamii ya
Nkungi na Vijiji Jirani, kutategemea aina ya msaada unaohitajika na uwezo wa
Chama; Aidha, kiasi halisi cha mchango kitapitishwa rasmi na Mkutano Mkuu wa
Chama. Ili kutekeleza azma hii, Chama
kitaanzisha mfumo rasmi wa mawasiliano na viongozi wa Nkungi na Vijiji Jirani
ili michango hiyo iweze kuwafikia walengwa kwa wakati.
16) WATEGEMEZI WANAOSTAHILI KUHUDUMIWA NA CHAMA
Wategemezi wa mwanachama (Mume/Mke) ni hawa wafuatao:
a)
Baba/Mama mzazi wa Mwanachama;
b)
Wakwe wa pande zote mbili za Mwanachama;
c)
Watoto rasmi wa mwanachama wasiozidi wanne;
d)
Aidha, mume mwenye wake zaidi ya mmoja, ni mke rasmi mmoja
tu atahesabika kuhudumiwa na chama; na
e)
Mwanaume au mwanamke ambaye hajaoa/hajaolewa
atahesabika kama mwanachama mmoja.
17) UKOMO WA UONGOZI
Kiongozi
anaweza kuondolewa uongozi wake kwa:
a)
Kutotimiza masharti ya uanachama;
b)
Kutohudhuria mikutano mitatu mfululizo bila taarifa;
c)
Kujiuzulu yeye mwenyewe kwa kuacha uanachama; na
d)
Kifo.
18) KUKOMA UANACHAMA
a)
Kwa ridhaa yake mwenyewe kwa kutoa taarifa ya
maandishi/maelezo mbele ya mkutano wa wanachama;
b)
Kwa kutotimiza masharti na taratibu za Chama;
c)
Kutoshiriki katika mikutano mitatu mfululizo ya chama bila
taarifa;
d)
Utovu wa nidhamu kwa wanachama wengine;
e)
Kutolipa ada ya kila mwezi kwa miezi mitatu mfululizo na
pia kutolipa michango mingine mfululizo kwa miezi mitatu bila taarifa kwa
uongozi;
f)
Endapo mwanachama ameshindwa kutimiza masharti yote ya
uanachama (Aya Na 9, 17, 18-c,d,&e), Chama kitalazimika kumfukuza uanachama
bila kurejeshewa hisa zake; na
g)
Kwa kufariki.
19) KUHAMA KWA WANACHAMA
a) Endapo
mwanachama atahama kwenda mkoa mwingine kikazi/kuishi, atarudishiwa michango
yake lakini atakatwa asilimia 50 ya akiba yake ili fedha zitakazobaki ziendeshe
shughuli za wanachama waliobaki;
b) Endapo
mwanachama atahama kwenda mkoa mwingine kikazi na kuamua kuendelea kuwa
mwanachama hai, kipengele 17 (b) na 18 (c) havitamhusu na atatakiwa kutimiza
masharti mengine yote ya uanachama.
20) MABADILIKO YA KATIBA
Katiba inaweza kufanyiwa
marekebisho kwa kupitishwa na zaidi ya asilimia 50 ya wanachama wote.
21) KUVUNJIKA KWA CHAMA
a)
Chama kinaweza kuvunjika endapo ni dhahiri hakuna
maelewano na zaidi ya asilimia 50 ya wajumbe wamedhamiria kukivunja chama;
b)
Maamuzi ya kuvunja Chama sharti yaafikiwe na Mkutano
Mkuu wa Chama kwa kuzingatia Kanuni za Chama; na
c)
Mgawanyo wa michango utafanyika kwa kuzingatia hisa
pamoja na michango mingine ambayo alichangia mwanachama.
DAR ES SALAAM, TANZANIA.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni